SABABU ZA KUPIMA VVU
Menu
MWANZO
15/6/2018
Hizi ndizo sababu kuu za wewe kutakiwa kwenda kupima VVU
By Peter Elias, Mwananchi pelias@mwananchi.co.tz
ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT
Kila mtu hayuko salama. Siyo mtoto wala mtu mzima, wote wako hatarini. Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) hayachagui. Yapo kila kona na mtu yeyote anaweza kuyapata kwa njia tofauti hasa ngono zembe kwa vijana.
Hata hivyo, waliopata maambukizi hayo wanapata dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs) ili waishi muda mrefu.
Pamoja na kupatikana kwa dawa hizo, bado kinga ni muhimu kuliko tiba na kila mtu ana nafasi ya kujikinga na maambukizi hayo.
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inafanya kila jitihada ili kutokomeza ugonjwa wa ukimwi hapa nchini. Vita hiyo itafanikiwa kama kila mmoja atajua hali yake na kuzingatia kanuni bora za afya kulingana na hali.
Anayebainika kuwa na maambukizi atapata ushauri na dawa za ARVs bure, atazingatia lishe bora na atajiepusha kushiriki ngono zembe ili asipate maambukizi mapya na yeye kuambukiza wengine.
Kadhalika, mtu ambaye atabainika kutokuwa na maambukizi hayo baada ya kupima, ataendelea kujikinga zaidi na kuelimisha watu wengine wanaomzunguka kusudi waepuke kuambukizwa ugonjwa huo ambao mpaka sasa hauna kinga wala tiba.
Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP) imeazimia kuwa ifikapo mwaka 2020, asilimia 90 ya Watanzania wawe wamepima na kujua afya zao, jambo ambalo litarahisisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Kwa kushirikiana na wadau kama vile Mfuko wa Ukimwi kwa Watoto wa Elizabeth Glaser, PEPFAR, USAID, Chuo Kikuu cha Maryland na Unicef, Serikali itaongeza hamasa ya upimaji wa ukimwi kwa wananchi wake.
Kila mtu katika familia anatakiwa kupima virusi vya ukimwi bila kujali umri wake.
Lakini Je changamoto iko wapi?
Changamoto katika upimaji huo inaelezwa ni kwa upande wa wanaume na kundi la vijana balehe ambao wana miaka kati ya 15 hadi 24.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Leonard Subi anasema ripoti ya maambukizi ya ukimwi ya mwaka 2016/17, inaonyesha maambukizi mapya kwa vijana balehe yalikuwa ni asilimia 26.
Anasema ripoti hiyo inaonyesha asilimia 65 ya wavulana hawajui hali zao wakati wasichana wakiwa ni asilimia 59 pekee.
Hivyo, Dk Subi anasema kundi hilo linahitaji elimu na msukumo mkubwa wa kupima.
“Takwimu zinaonyesha asilimia 12 ya vijana balehe wameanza kufanya ngono wakiwa na miaka 15 na matumizi ya kondomu kwa vijana hao yako chini sana,” anasema Dk Subi na kusisitiza kwamba, kundi hili likijua hali zao, jamii nzima itakuwa katika nafasi nzuri ya kutopata maambukizi.
Amewataka wadau wa masuala ya ukimwi kuongeza nguvu na kuhakikisha kila mwananchi anajua afya yake hasa kwa kundi kubwa la vijana wanaobalehe na kuingia kwenye vitendo vya ngono bila kuchukua tahadhari.
Anatoa wito pia kwa wanaume kujitokeza kupima afya kwa sababu takwimu zinaonyesha wengi wao hawapimi.
Anasema kwa sasa, inaonyesha zaidi ya asilimia 90 ya wanawake hujitokeza kupima virusi vya ukimwi kila wanapokwenda kliniki.
Dk Subi anawahimiza wananchi kutumia fursa ya vituo vya afya 6,259 vilivyopo nchini kupima afya zao na kupatiwa tiba pale wanapobainika kuwa na maambukizi ya ukimwi.
Pia, anawahimiza walio na maambukizi kuhudhuria kliniki za huduma na tiba (CTC) mara kwa mara.
Mkurugenzi huyo anawashauri wazazi wakae na vijana wao wawapatie elimu ya maambukizi ya VVU na kama wao wamewaambukiza, basi wawajulishe mapema ili wachukue tahadhari na kuepusha maambukizi kwa wengine. “Mwaka ujao tunataka kufikia lengo la asilimia 90 kwenye maambukizi ya ukimwi kwa watoto na vijana balehe. Ifikapo mwaka 2030 tunataka ukimwi uwe umekwisha hapa nchini,” anasema mtaalamu huyo wa afya.
Hali ikoje kwa nchi zingine
Tatizo la maambukizi kwa watoto na vijana balehe halipo nchini pekee, ni tatizo la ulimwengu wote. Nchi mbalimbali nazo zinakabiliwa na maambukizi kwa rika la vijana wadogo wanaojiingiza kwenye ngono zembe bila kutumia kinga.
Kiongozi wa kitengo cha ukimwi cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), Dorothy Ngacha anasema ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Ukimwi (Unaids), inaonyesha watoto milioni 2.1 wanaishi na virusi vya ukimwi duniani.
Anasema kundi kubwa la watoto hao wanatoka Bara la Afrika na Tanzania ni miongoni mwa nchi kumi ambazo zina maambukizi makubwa ya VVU kwa watoto wenye miaka 0 hadi 14.
Nchi nyingine ni Afrika Kusini, Nigeria, Msumbiji, Uganda, India, Kenya, Malawi, Zambia na Zimbabwe.
Anasema ripoti hiyo inaonyesha vifo vya watoto vitokanavyo na ukimwi katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika ni 30,000 wenye umri wa miaka 0 hadi 4, kati yao, wasichana ni 15,000 na wavulana ni 15,000.
Wenye umri wa miaka 5 hadi 9 ni wasichana 6,100 na wavulana 6,500 wakati wenye miaka 10 hadi 14, wakike ni 8,100 na wavulana 8,500.
Kadhalika, wenye miaka 15 hadi 19, wasichana 7,900 na wavulana 9,000. Wenye miaka 20 hadi 24 ni wasichana 12,000 na wavulana 7,800.
“Ili kupunguza maambukizi mapya kwa watoto wenye miaka 0 hadi 14, tunatakiwa kufanya kazi na majukwaa ya kijamii na kutambua watoto ambao hawajapimwa, kisha kuwaunganisha kwenye mfumo wa afya,” anasema Ngacha.
Anasema watoto wanatakiwa kupimwa VVU miezi miwili baada ya kuzaliwa kama inavyoshauriwa.
Anabainisha kwamba ni muhimu pia kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za afya ili kuwatambua mama wanaoishi na VVU hasa wale wenye umri mdogo.
Hali ya maambukizi nchini
Utafiti wa Athari za maambukizi ya VVU nchini (THIS) wa mwaka 2016/17 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), unabainisha kwamba vichocheo vya maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 ni asilimia 0.26 ambayo ni sawa na maambukizi mapya 81,000.
Utafiti huo wa NBS unabainisha kwamba, watu wenye VVU walio na umri wa miaka 15 hadi 64 hapa nchini ni asilimia 5 (asilimia 6.5 wakiwa ni wanawake na asilimia 3.5 wanaume) ambayo ni sawa na watu milioni 1.4.
Kwa mujibu wa utafiti huo, viwango vya maambukizi ya VVU kwa watu wenye miaka 15 hadi 64 vinatofautiana kijiografia hapa nchini.
Kiwango cha juu ni asilimia 11.4 katika Mkoa wa Njombe na kiwango cha chini ni asilimia Moja katika Mkoa wa Lindi na Zanzibar.
Mikoa mingine yenye viwango vya juu ni Mbeya (asilimia 9.3), Mwanza (asilimia 7.2), Kagera (asilimia 6.5), Shinyanga (asilimia 5.9) na Katavi (asilimia 5.9).
mikoa yenye viwango vya chini ni Lindi (asilimia 0.3), Arusha (asilimia 1.9), Mtwara (asilimia 2), Manyara (asilimia 2.3) na Kilimanjaro (asilimia 2.6).
Ripoti hiyo inabainisha kwamba mpango wa 90-90-90 unaolenga kumaliza maambukizi ya ukimwi kwa kufikia asilimia 90 ya watu wenye VVU kujua hali zao, wenye VVU kupata dawa na hao wanaopata dawa kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.
Kwa mujibu wa utafiti huo wa mwaka 2016/17, asilimia 52 ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wenye umri wa miaka 15 hadi 64 ndiyo wanajua wana VVU. Asilimia 90 ya wenye VVU wanatumia dawa za ARVs.
Binti mwenye VVU afunguka
Suhaila Msham (19) ni msichana anayeishi na VVU na hapa anabainisha changamoto wanazopitia kuwa ni pamoja na shule nyingi za binafsi huko Zanzibar anakoishi hazitoi elimu ya VVU na ukimwi kwa wanafunzi.
Anatoa rai kwa Serikali kuweka utaratibu ambao utazisukuma shule kutoa elimu hiyo kwa vijana ili watambue namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU.
Anasema wazazi pia wawaelimishe watoto wao kuhusu suala hilo.
Anasema vijana wengi wa umri wake walio na VVU wanakabiliwa na lishe duni kwa sababu wengi wao wanaishi na mzazi mmoja, jambo linalowafanya washindwe kumudu lishe bora wakati wote.
Suhaila anaiomba Serikali iweke utaratibu kwa wenye virusi vya ukimwi kunywa dawa angalau mara moja kwa mwezi kwa sababu kunywa dawa kila siku kunachosha na wakati mwingine wapo wanaosahau kuzinywa.
“Unyanyapaa katika jamii bado upo lakini watu watambue kuwa na virusi vya ukimwi siyo mwisho wa maisha, tunaweza kutimiza ndoto zetu,” anasema binti huyo aliyeambukizwa VVU na wazazi wake ambao walifariki dunia akiwa na miaka tisa.
Maoni
Chapisha Maoni